Jumla ya Mara Iliyotazamwa

13 Sep 2014

TMF YATOA SHS. 1.7 BILIONI KWA VYOMBO VYA HABARI


Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura

NA BEATRICE SHAYO


Katika kuendeleza habari za uchunguzi nchini Mfuko wa vyombo vya habari (TMF) umetoa ruzuku ya Sh. bilion 1.7 kwa vyombo vya habari 16.
Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura, alisema jana wakati wa kutia saini mkataba wa mwisho wa kutekeleza makubaliano ya kufanya habari za uchunguzi nchini.
Sungura alisema ruzuku hiyo inatakiwa kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba wamewaweka wakaguzi wao wa ndani watakaokagua mara kwa mara. 
“Ruzuku hiyo imetokana na msaada wa kodi za wananchi kutoka nchi za Denmark, Swissland, Norway na Uingereza kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo hivyo inatakiwa kuzithamini na kuweka nidhamu kubwa,” alisema.
Sungura alisema, kwa atakaye fuja au kutumia vibaya ruzuku hiyo atakuwa anajitafutia ubaya na kwamba hatapata tena nafasi ya kupata ruzuku hiyo ambayo hutolewa kila mwaka.
Aidha, alisema jamii ipo katika changamoto kadhaa hali ambayo inasababisha maisha ya watu kutobadilika, vyombo vya habari vinatakiwa kuliangalia suala hilo katika kuibua mambo mbalimbali ili kuwepo na mabadiliko.
Alisema mahitaji muhimu ya binadamu hayapatikani katika jamii ikiwamo huduma za afya, shule na vitu vingine vya muhimu vimekuwa havipatikani kutokana na changamoto za tabia za kibadhirifu.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari vinahesabiwa kuwa ni muhimili ambao siyo rasmi wakati ni muhimili muhimu unaofanya kazi kubwa na kuibua mambo mbalimbali yakiwamo ya ufisadi.
Aidha, alisema mkakati wao ni kuendelea kuviwezesha vyombo vya habari katika kuibua maovu ndani ya jamii, ili changamoto hizo ziweze kufanyiwa kazi.
Ruzuku hiyo imegawanywa katika makundi mbalimbali na kwamba chombo cha habari kilichopata ruzuku kubwa ni Sh. milioni 185 na cha mwisho kimepata Sh. milioni 50.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni