MADAI mazito! Super
lady wa sinema za Kibongo, Ruth Suka ‘Mainda’ anadaiwa kugombana na
muumini mwenzake kwenye kanisa analoabudu kwa sasa, Amani limedokezwa.
TUJIUNGE NA MTOA HABARI
Kwa mujibu wa chanzo makini, tukio hilo la aina yake lilijiri kwenye
kanisa hilo la kiroho lililopo chini ya mchungaji wake aliyetajwa kwa
jina moja la Mwamposa, Sinza-Lion jijini Dar, Jumapili iliyopita.
Mtu mmoja aliyedai anaabudu kwenye kanisa hilo linalokuja juu kwa sasa,
akizungumza Jumapili usiku kwa simu ya chumba cha habari cha Global
Publishers, alisema Mainda alitofautiana na mwenzake (jina
halikupatikana mara moja) wakati wakifanya usafi kama sehemu ya huduma
yao kanisani hapo. “Jamani niwape habari, leo hapa kwenye kanisa la
Mchungaji Mwamposa, Sinza-Lion, Mainda amegombana na muumini mwenzake
kisa kikiwa ni kiti tu.
“Mainda alikuwa akisafisha viti ili aviingize kwa mchungaji huyo,
mwenzake akaja na kukalia. Akaja juu, yule naye akaja juu! Acha
wagombane,” alisema mtu huyo.
AMANI MZIGONI
Baada ya kudakishwa madai hayo, Amani liliingia mzigoni ili kupata
undani ambapo mambo yalikuwa hivi; JUMATATU, SAA 4:00 ASUBUHI Kwa kuwa
tukio lilidaiwa kujiri Jumapili, Jumatatu saa 4:00 asubuhi, mwanahabari
wetu alifika kanisani hapo na kufanya ‘ushushushu’ kabla ya
kujitambulisha kuwa anatoka Global Publishers.
MUUMINI
Akielezea tukio hilo kwa undani zaidi, mmoja wa waumini ambaye hakutaka
kutaja jina lake alidai tukio hilo lilitokea jana yake (Jumapili) wakati
watumishi hao wakifanya usafi wa kawaida. Alidai kuwa, Mainda alikuwa
akifuta vumbi kwenye viti ili aviingize kwa mchungaji, mara mwenzake
akaja na kukalia kimojawapo na ndipo wakaanza kurushiana maneno.
“Wao ndiyo watenda kazi humu ndani, sasa unakuta labda mtu anamuagiza
mwenzake amletee kitu fulani lakini anakataa. “Ninavyojua mimi ni
kwamba, Mainda alikuwa akifuta viti na kuvipeleka ndani kwa mchungaji,
mara mwenzake akaja na kukaa pale, wakaanza kuzozana: Lete kiti...wee
unaona mimi nafuta ili viingie kwa mchungaji, wewe unakuja kukalia,”
alisema mtumishi huyo akichukuliwa (kurekodiwa) sauti kwa sharti la
kutotajwa popote.
MUUMINI MWINGINE
Muumini mwigine aliyekuwa eneo hilo naye alidakia huku akirekodiwa: “Ni
kweli waligombana lakini baadaye waliwekwa chini na kumaliza tofauti zao
na wote wanaendelea kutoa huduma kama kawaida. Watu wa Mungu
hawawekeani visasi hata siku moja.”
MZEE MUUMINI
Baada ya kupata maelezo hayo, gazeti hili lilimfuata mzee mmoja
aliyekuwa kanisani hapo muda huo ambaye hakutaka kutaja jina lake ambapo
alikiri kuwepo kwa ugomvi wa Mainda na mwenzake huku akisisitiza kisa
kilianza kwenye kiti. Alisema baadaye walisuluhishwa na wakapatana mambo
mengine yakaendelea kwa amani. “Jamani hata hili jambo dogo limewafikia
hadi ninyi? Hii sasa ni hatari! Waligombana kweli lakini waliwekwa sawa
wakapatana.Kisa
ni kiti tu, Mainda kakifuta ili akiingize kwa mchungaji mwenzake akaja
kukikalia, hilo ndiyo tatizo,” alisema mzee huyo bila kutaja nafasi yake
ya huduma katika kanisa hilo. Akaendelea: ”Kukwaruzana ni jambo la
kawaida katika sehemu yenye mkusanyiko wa watu kama hapa, hasa kwa
wasichana kama hawa.” Mwanahabari wetu alipotaka kuzungumza na
Mchungaji Mwamposa kama anajua lolote juu ya sakata hilo, aliambiwa
kiongozi huyo yupo safirini kwa huduma ya kiroho.
MAINDA HEWANI
Baada ya kutoka kwenye kanisa hilo, mwandishi wetu alimtwangia simu
Mainda ambapo alipopatikana alisema: “Siyo kweli. Mimi sijui chochote.
Kama unataka uje kanisani uongee na wachungaji.” Baada ya kukata simu na
kupita dakika kadhaa, Mainda alipiga simu kwa mwanahabari wetu na
kutaka kumjua ni nani aliyezifikisha habari hizo Global Publishers.
Alijibiwa si maadili ya kazi kutaja chanzo cha habari. JUMATATU SAA
10:00 JIONI Siku hiyohiyo, mishale ya saa 10:00 jioni, gazeti hili
lilirudi tena kanisani hapo ili kuzungumza na wachungaji kama alivyotaka
Mainda ambapo lilibahatika kukutana na muumini aliyesema yeye ni mzee
wa kanisa lakini akagoma kutaja jina lake.
Mzee huyo alisema hajui lolote na kwamba kama ni kugombana kwa watu kupo
lakini kuhusu Mainda hakutaka kuzungumzia lolote. Kwa bahati nzuri,
muda huo Mchungaji Mwamposa ambaye ndiyo alikuwa amerejea kutoka
safarini alikuwepo, Hata hivyo, alikataa kuzungumza chochote kwa kuwa
hakuwepo. “Mimi sikuwepo hivyo siwezi kuongea chochote maana sijaambiwa
chochote,” alisema Mwamposa.
MUUMINI AHOFIA
Wakati mwandishi wetu anatoka nje ya kanisa hilo, alimuuma sikio muumini
mmoja akimtaka amtajie jina la muumini aliyegombana na Mainda, lakini
akasema: “Wewe ni mwandishi wa habari! Akha! Kama unataka huduma ya
kiroho nitakusaidia lakini si hayo mengine, naogopa mwaya.”
KAMA ZALI, MAINDA HUYU!
Baada ya kumsikia muumini huyo, mzee wa kanisa na baba mchungaji, kama
zali ghafla Mainda alitokea ambapo kwa upande wake, alikanusha tena
madai hayo na kusema kuwa haelewi chochote kuhusiana na ugomvi huo.
“Nashangaa kusikia hivyo na sijui chochote kuhusu hilo, kawaulize vizuri
haohao waliokwambia,” aliwaka Mainda.
MNYONGE MNYONGENI, HAKI YAKE...
Pamoja na yote lakini Mainda anakuwa msanii nyota Tanzania ambaye
amedumu katika mazingira ya kumtumikia Mungu tangu akate shauri la
kuokoka takribani miaka miwili iliyopita. Amekuwa mstari wa mbele
kuusimamia wokovu wake kwa dhati, akihudumu kanisani hapo kwa kufanya
usafi asubuhi na jioni bila kukosa ibada.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni